Nenda kwa yaliyomo

Malipizi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Malipizi (kutoka kitenzi "kulipa") ni matendo yanayofanywa ili kufidia hasa makosa na madhara.

Katika Ukristo

[hariri | hariri chanzo]

Neno hilo linatumika sana katika Ukristo kuhusu kufidia dhambi[1], kama vile kwa kukamilisha sakramenti ya kitubio.

Katika dini hiyo inaeleweka kwamba malipizi kamili ni yale ya Yesu msalabani[2].

Mkristo yeyote anapaswa kubeba “msalaba wake kila siku” (Lk 9:23) na kuunganisha mateso yake na sadaka ya Yesu inayozidi kutolewa altareni: anapaswa kuyatoa kwa ajili yake na ya watu anaoshughulikia wokovu wao. Kwa mfano wa Bikira Maria, mabibi arusi wengi wa Kristo wanashiriki mateso yake na hivyo kuwa mama wa Kiroho kwa wale wote waliokombolewa na damu ya Mwanae. Maria hakutiwa rohoni alama isiyofutika ya upadri lakini “alijaliwa ukamilifu wa roho ya kipadri” (M. Olivier) yaani roho ya Mkombozi. Alipenya fumbo la altareni kuliko Mtume Yohane aliyeadhimisha misa mbele yake na kumkomunisha. Alistawisha utume wa Thenashara akijitoa pamoja na sadaka ya misa. Kwa mateso yake ya ndani, kama yale yaliyompata uzushi ulipoanza kujitokeza, alikuwa mama wa Kiroho wa watu kwa kiwango kisichofikirika pasipo mang’amuzi ya dhati ya utume huo uliofichika. Kwa namna hiyo aliendeleza sadaka ya Mwanae.

“Mwili wa fumbo wa Kristo hauwezi kuishi pasipo mateso, kama vile macho yetu yasivyoweza kuishi bila mwanga wa jua. Hapa chini kadiri mtu alivyo karibu na Mungu, yaani kadiri anavyompenda, anawekwa wakfu kwa mateso. Kwa watu waliopata yote kwa njia ya Kanisa, je, si wito bora kuishi na kujitoa sadaka kwa ajili ya Mama yao?… Inahitajika subira, lakini nitaipata: Bwana wetu atanipatia… Namuambia daima: ‘Namtaka mtu huyu kwa gharama ya mateso yoyote’… Hadi mwisho wa dunia Kristo atateseka katika viungo vyake, na kwa mateso hayo Kanisa, Bibi arusi wake, litazaa watakatifu… Tangu Yesu afe, sheria haijabadilika: watu wanaokolewa tu kwa kuteseka na kufa kwa ajili yao… Moyo wa Yesu uliotukuzwa milele hautateseka tena kwa sababu hauwezi kuteseka tena. Sasa ni zamu yetu… Ni heri iliyoje kwamba kuteseka ni zamu yetu, si zamu yake tena!” (Fransiska wa Yesu).

Bwana anawaambia watu wa malipizi kama sista huyo aliyeishi miaka kadiri ya kweli hizo, “Je, hujaniomba kushiriki mateso yangu? Chagua: unataka furaha ya imani isiyo na vivuli, ambayo ikupate na kukujaza matamu, au unataka giza na uchungu ili uchangie kuokoa watu?” Anawaalika waamue kwa hiari tu; lakini wao, wakivutwa na nguvu isiyoshindikana, wanajichagulia uchungu na giza lote ili wengine wapewe mwanga, utakatifu na wokovu. Pengine Bwana anawaonyesha ugumu wa mioyo, na ni kana kwamba mashetani wote wanajaribu kwa kila namna kuwakatisha tamaa; kwa saa kadhaa wanapambana nao roho kwa roho ili kumfuata kwa vyovyote Mwalimu mwema mpaka mwisho. Naye anawajalia kuelewa zaidi na zaidi anavyotarajia wapende kudharauliwa na kuangamia, kama chembe ya ngano iliyomwagwa ardhini ioze ikazae kwa wingi.

Ndiyo dalili ya upendo kamili ambao “unatolewa na Roho Mtakatifu akiushirikisha utashi nguvu yake mwenyewe” (Katerina wa Siena). Bwana alimuambia mtakatifu huyo kuwa wanaotamani wokovu wa watu “hawana lengo lingine isipokuwa kuteseka na kukabili uchovu wowote kwa manufaa ya jirani, wakichukua mwilini mwao madonda ya Kristo, kwa kuwa upendo msulubiwa unaowajaa unajitokeza katika kujidharau, kufurahi kudhalilishwa, kupokea mapingamizi na mateso mengine ninayowajalia toka pande zote na kwa namna yoyote… Hivyo wanalingana na Mwanakondoo asiye na doa, Mwanangu pekee ambaye msalabani alikuwa na heri na uchungu kwa wakati mmoja… Nani anaweza kuninyang’anya na kusogeza mbali nami watu hao, waliozama katika moto wa upendo, kwa kutokuwa na matakwa yoyote ya kwao tena na kwa kuwaka kabisa kwa ajili yangu?”

Ndio ulinganifu kamili na Yesu Kristo unaozaa na kuangaza katika maisha ya malipizi. Hata kwa wasiopokea upadri ni kushiriki hali ya kafara ya Yesu na kuungana kwa dhati na kuhani wa milele: “Mmwendee yeye, jiwe lililo hai, lililokataliwa na wanadamu, bali kwa Mungu ni teule, lenye heshima. Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo” (1Pet 2:4-5).

  1. Pope Pius XI, "Miserentissimus Redemptor", §6, Libreria Editrice Vaticana
  2. Kilmartin, Edward J. (1999). The Eucharist in the West, History and Theology. Collegeville, MN: Liturgical Press. ku. 381f. ISBN 0814661726. See also Robert Daly, “Sacrifice Unveiled or Sacrifice Revisited”. Theological Studies, March 2003 and Walter Kasper, The God of Jesus Christ. Crossroad (1986), pp. 191,195. ISBN|0824507770.
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Malipizi kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.