,

Meksiko Quotes

Quotes tagged as "meksiko" Showing 1-11 of 11
Enock Maregesi
“Usiwe na wasiwasi, Peter. Hizo ni hisia zangu tu. Huwezi kuwa mpelelezi. Lakini, kusema ule ukweli, ningependa sana kuonana na John Murphy. Kuna kazi binafsi ningependa kumpa. Wewe unatoka Afrika, hujawahi kumwona?” Debbie alizidi kumshtua Murphy.
“Nani?” Murphy aliuliza huku akitabasamu.
“John Murphy wa Afrika.”
“Sijawahi kumwona. Mbona unamuulizia hivyo?”
Debbie alitulia. Kisha akarusha nywele ili aone vizuri.
“Nampenda sana!”
“Kwa nini?”
“Simpendi kwa mahaba, lakini.”
“Ndiyo. Kwa nini?”
“OK. Nampenda kwa kipaji chake. Alichopewa na Mungu, cha ujasusi. Kusaidia watu.”
“Ahaa!” Murphy alidakia, sasa akifikiri sana.
“Murphy ana mashabiki wengi hapa Meksiko bila yeye mwenyewe kujua, kwa sababu ya kupambana na wahalifu wa madawa ya kulevya – hasa wa huku Latino. Tatizo lake haonekani. Wengi hudhani ni hadithi tu, kwamba hakuna mtu kama huyo hapa duniani.”
“Hapana! Murphy yupo! Ni mfanyabiashara maarufu huko Tanzania. Lakini ndiyo hivyo kama unavyosema ... Haonekani!”
Enock Maregesi, Kolonia Santita

Enock Maregesi
“Mpenzi. Sikiliza. Magaidi yaliyomuua Marciano yana mtandao dunia nzima na watu wote wanayajua. Yanaitwa Kolonia Santita. Tatizo hata hivyo ni moja: Hakuna mtu amewahi kuthibitisha au kutoa ushuhuda wa uhalifu wao ili watiwe nguvuni. Huendesha maisha yao kibabe na yana kila mbinu ya kukwepa sheria, ndani na nje ya Meksiko. Watu wengi wameuwawa kwa sababu ya Kolonia Santita. Ukileta kidomodomo yanakuua; au yanakupa notisi ya kuhama mji au nchi, ukakae mbali na Meksiko au Mexico City.”
Enock Maregesi, Kolonia Santita

Enock Maregesi
“Majambazi huwapenda wanaowapenda. Chukulia mfano huu: Mimi na Wanda ni marafiki, OK? Baba yake, au genge la baba yake, hataweza kunidhuru au kuwadhuru watu ninaowapenda kwa sababu tu ya urafiki na mtoto wake. Na yeye anaweza kufumbiwa macho akifanya makosa kwa sababu mimi na mtoto wake ni marafiki wakubwa. Murphy, hapa Meksiko tuna kitu kinaitwa Bima ya Utekaji Nyara ('Ransom Insurance'). Zamani nilikuwa nalipa dola milioni kumi za Marekani kama bima ya utekaji nyara; Lisa alikuwa analipa milioni nne na Wanda bado analipa milioni mbili mpaka sasa hivi. Baada ya mimi na Lisa kujenga urafiki na Wanda, malipo yetu ya bima yamepungua mpaka dola milioni moja kwa mwaka.”
Enock Maregesi, Kolonia Santita

Enock Maregesi
“Peter, naomba nitubu kosa. Mimi si mtoto wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Ni mtoto wa Rais wa Meksiko. Lisa ni mtoto wa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali,” Debbie alisema akitabasamu.
“Hata mimi nilijua ulikuwa ukinidanganya. Lakini mbona Rais wa Meksiko haitwi Patrocinio Abrego?” Murphy aliuliza.
“Utamaduni wa Meksiko ni tofauti kidogo na tamaduni zingine,” Debbie alijibu baada ya kurusha nywele nyuma kuona vizuri. “Hapa, watu wengi hawatumii majina ya pili ya baba zao. Hutumia jina la kwanza la mama la pili la baba; ndiyo maana Wameksiko wengi wana majina matatu. Kwa upande wangu, Patrocinio ni jina la baba yake mama yangu na Abrego ni jina la babu yake mama yangu – kwa sababu za kiusalama.”
Enock Maregesi, Kolonia Santita

Enock Maregesi
“Kamishna … karibu," alisema Nafi huku akisimama na kutupa gazeti mezani na kuchukua karatasi ya faksi, iliyotumwa.
"Ahsante. Kuna nini …"
"Kamishna, imekuja faksi kutoka Oslo kama nilivyokueleza – katika simu. Inakutaka haraka, kesho, lazima kesho, kuwahi kikao Alhamisi mjini Copenhagen," alisema Nafi huku akimpa kamishna karatasi ya faksi.
"Mjini Copenhagen!" alisema kamishna kwa kutoamini.
"Ndiyo, kamishna … Sidhani kama kuna jambo la hatari lakini."
"Nafi, nini kimetokea!"
"Kamishna … sijui. Kwa kweli sijui. Ilipofika, hii faksi, kitu cha kwanza niliongea na watu wa WIS kupata uthibitisho wao. Nao hawajui. Huenda ni mauaji ya jana ya Meksiko. Hii ni siri kubwa ya tume kamishna, na ndiyo maana Oslo wakaingilia kati."
"Ndiyo. Kila mtu ameyasikia mauaji ya Meksiko. Ni mabaya. Kinachonishangaza ni kwamba, jana niliongea na makamu … kuhusu mabadiliko ya katiba ya WODEA. Hakunambia chochote kuhusu mkutano wa kesho!"
"Kamishna, nakusihi kuwa makini. Dalili zinaonyesha hali si nzuri hata kidogo. Hawa ni wadhalimu tu … wa madawa ya kulevya."
"Vyema!" alijibu kamishna kwa jeuri na hasira. Halafu akaendelea, "Kuna cha ziada?"
"Ijumaa, kama tulivyoongea wiki iliyopita, nasafiri kwenda Afrika Kusini."
"Kikao kinafanyika Alhamisi, Nafi, huwezi kusafiri Ijumaa …"
"Binti yangu atafukuzwa shule, kam …"
"Nafi, ongea na chuo … wambie umepata dharura utaondoka Jumatatu; utawaona Jumanne … Fuata maadili ya kazi tafadhali. Safari yako si muhimu hivyo kulinganisha na tume!"
"Sawa! Profesa. Niwie radhi, nimekuelewa, samahani sana. Samahani sana.”
Enock Maregesi, Kolonia Santita

Enock Maregesi
“Meli ya kwanza kuondoka katika Bandari ya Salina Cruz kusini mwa Meksiko katika Bahari ya Pasifiki ni 'La Diosa de los Mares', 'Mungu wa Bahari', au 'Goddess of the Seas', Tani 6000, iliyoondoka saa tisa kamili usiku kuelekea Miami nchini Marekani; wakati ya mwisho kuondoka ilikuwa CSS ('Colonia Santita of the Seas', Tani 10000), na SPD ('El Silencio Depredador del Profundo', 'Mnyama Mtulivu wa Kina Kirefu', 'The Silent Predator of the Deep' – nyambizi ya Panthera Tigrisi), zilizoondoka saa kumi na moja alfajiri kuelekea Guatemala na Kolombia. Salina Cruz ni sehemu iliyopo kandokando mwa Bahari ya Pasifiki kusini kabisa mwa Meksiko na kaskazini-mashariki kwa Reparo Jicara katika jimbo la Oaxaca. Kambi ya Panthera Tigrisi ilijengwa ndani ya Msitu wa Benson Bennett – katika ufuko wa bahari kubwa kuliko zote ulimwenguni, iliyopuliza hewa na kuyumbisha miti anuai juu ya maabara kubwa kuliko zote katika Hemisifia ya Magharibi; ya kokeini, heroini, bangi, eksitasi na hielo ya China na Kolombia. Panthera Tigrisi alikamatwa katika Bahari ya Pasifiki. Kahima Kankiriho alikamatwa katika Msitu wa Bennett.”
Enock Maregesi

Enock Maregesi
“Kwa sababu za kijiografia, Copenhagen iko mbele kwa masaa 9 (PST) kuilinganisha na Tijuana (kaskazini-magharibi mwa Meksiko) na masaa 7 (CST) kuilinganisha na Salina Cruz (kusini-magharibi mwa Meksiko). Mauaji ya Meksiko yametokea saa 4 usiku wa Jumanne, Copenhagen ikiwa saa 1 asubuhi Jumatano CET. Saa 5 usiku wa Jumanne, El Tigre anahamishwa (na ndege binafsi) kutoka katika milima ya Tijuana (alikokuwa amejificha) mpaka katika jumba la kifahari la Eduardo Chapa de Christopher (Mkurugenzi wa Usafirishaji wa Kolonia Santita) nje ya Salina Cruz – ambako Chui anafika saa 10 alfajiri na kuendesha kikao cha dharura cha Bodi ya Wakurugenzi ya Kolonia Santita.”
Enock Maregesi, Kolonia Santita

Enock Maregesi
“Kolonia Santita imesambaa dunia nzima. Hapa Meksiko wana magenge rafiki zaidi ya mia moja yakiwemo makubwa kabisa katika Latino ya Matamolos na Baja California. Nikitekwa nyara na memba yoyote wa magenge hayo, kuna uwezekano mkubwa wasinifanye chochote au nisilipe chochote kwa sababu ya Wanda. Fadhila ya uhalifu. Kwa sababu ya fadhila ya uhalifu; baba, au viongozi wengine wa serikali ambao watoto wao wamo ndani ya 'mpango' huo, wanatakiwa wawakingie kifua (kwa namna yoyote wanayoweza) pindi wanapoanguka katika mikono ya dola na sheria. Wasipofanya hivyo kutakuwa na vita ya ndani kwa ndani … kama unanielewa. Hivyo, kuna mtu anaitwa El Tigre – baba yake Wanda – ndiye ninayetaka unisaidie. Amemuua Marciano, na watu wengi wa Meksiko. Nataka kumlipia kisasi Marciano, na marafiki zangu wengi ambao El Tigre amewaua, hata kwa njia isiyodhahiri.”
Enock Maregesi, Kolonia Santita

Enock Maregesi
“Kesho yake Ijumaa Rais wa Meksiko alirudi kutoka Panama na aliomba kuonana na Vijana wa Tume; alitaka kuwapongeza binafsi, na kuwapa nishani za heshima kwa mchango wao mkubwa kwa Jamii ya Meksiko. Randall Ortega alilipeleka ombi hilo kwa Rais wa Tume ya Dunia; Rais wa Tume ya Dunia akakaa na Kamati ya Usalama ya Tume ya Dunia na kumrudishia Randall Ortega jawabu, kwamba Vijana wa Tume waliruhusiwa kuonana na Rais wa Meksiko na baadhi ya maafisa wa juu wa serikali ya shirikisho. Saa mbili usiku wa siku hiyo, Ijumaa, kulifanyika sherehe ndogo ya siri nyumbani kwao Debbie; sherehe iliyohudhuriwa na Rais wa Meksiko na mke wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini Meksiko, Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya Nchini Marekani, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu Nchini Meksiko, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, maafisa wa tume na watu wengine wa muhimu katika kazi ya Vijana wa Tume.”
Enock Maregesi, Kolonia Santita

Enock Maregesi
“Wakiwa na suti nzito za kijani na madoa meusi (‘Ghillie Suits’) kwa ajili ya kupigania porini; Vijana wa Tume walikuwa na kofia za chuma, miwani ya kuonea usiku (iliyokuwa na uwezo wa kubinuka chini na juu), redio na mitambo ya mawasiliano migongoni mwao juu ya vizibao vya kuzuia risasi, vitibegi vya msalaba mwekundu (‘Blowout Kits’ – katika mapaja ya miguu yao ya kulia, ndani yake kukiwa na pisto na madawa ya huduma ya kwanza), vitibegi vya kujiokolea (‘Evasion Kits’ – katika mapaja ya miguu yao ya kushoto, ndani yake kukiwa na visu na pesa na ramani ya Meksiko) na bunduki za masafa marefu. Kadhalika, Vijana wa Tume waliamua kuchukua Punisher – waliyoafikiana baadaye kuwa ilikuwa nzuri kuliko RPG-7, ‘Rocket Propelling Gun’, ambayo Mogens alipendekeza waitumie kubomolea Kiwanda cha Dongyang Pharmaceuticals; kwa sababu hakutaka kuleta madhara kwa watu waliokuwa hawana hatia.”
Enock Maregesi, Kolonia Santita

Enock Maregesi
“Kofia za chuma au sandarusi zenye uwezo wa kukwepesha risasi za wadunguzi na kuzuia mpaka risasi tatu za AK-47, ijapokuwa zimetengenezwa kuzuia risasi moja tu, ni miongoni mwa vitu 17 vilivyobebwa na makomandoo wa Tume ya Dunia; wakati wakitekeleza Operesheni ya Kifo au Ushindi Kamili (operesheni ndogo ya Operation Devil Cross ya Tume ya Dunia) katika Msitu wa Benson Bennett, Salina Cruz, Oaxaca, nchini Meksiko. Thamani ya vitu vya komandoo mmoja wa EAC ('Executive Action Corps') akiwa vitani ni zaidi ya dola za Kimarekani 65,000; ikiwa ni pamoja na magwanda ya jeshi ('Ghillie Suits'), kofia za chuma, miwani ya kuonea usiku (yenye uwezo wa kubinuka chini na juu), redio na mitambo ya mawasiliano migongoni mwao juu ya vizibao vya kuzuia risasi, vitibegi vya msalaba mwekundu ('Blowout kits' – katika mapaja ya miguu yao ya kulia, ndani yake kukiwa na pisto na madawa ya huduma ya kwanza), vitibegi vya kujiokolea ('Evasion Kits' – katika mapaja ya miguu yao ya kushoto, ndani yake kukiwa na visu na pesa na ramani ya Meksiko) na bunduki za masafa marefu.”
Enock Maregesi